Akizungumza na vyombo vya habari, Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Ulaya Ursula von der Leyen amesema kuwa, ushuru mkubwa uliowekwa na rais wa Marekani Donald Trump ni pigo kubwa kwa uchumi wa dunia na amesisitiza kuwa Umoja wa Ulaya utajibu kivitendo hatua hizo za Trump ikiwa mazungumzo yatashindwa.
"Tayari tunakamilisha kifurushi cha kwanza cha hatua za kukabiliana na ushuru wa chuma," amesema Ursula von der Leyen kwenye taarifa iliyosomwa katika mji mkuu wa Uzbekistan jana Alkhamisi, kabla ya Mkutano wa Ushirikiano wa EU na Asia ya Kati.
Ameongeza, "Sasa tunajiandaa kwa hatua zaidi za kulinda maslahi na biashara zetu Ulaya, kama mazungumzo yatashindwa."
Kwa upande wake, Waziri Mkuu mpya wa Canada, Mark Carney amesema kwamba ushuru wa serikali ya Trump hauilengi tu Canada bali pia uchumi wa dunia nzima.
Amesema: "Ushuru wa Trump ni janga hivyo fungate ya uhusiano wa kina kati yetu na Marekani imekwisha."
Waziri Mkuu wa Canada amesisitiza kuwa nchi hiyo itapambana kivitendo na ushuru wa Marekani hadi utakapoondolewa.
Waziri Mkuu wa Canada pia amesema, nchi yake imefanya mazungumzo mazuri na Mexico na nchi za Umoja wa Ulaya pamoja na pande nyinginezo ili kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kupambana na Marekani.
342/
Your Comment